Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alitembelea Madrasat Imam Shahid, iliyopewa jina la Ayatullah Al-Udhma Khamenei (r.a.), mjini Qum, ambapo alikagua vitengo mbalimbali vya madrasa hiyo. Aidha, alipokea taarifa kuhusu mwenendo wa shughuli za kielimu, kitaaluma na kiutamaduni, na kutoa maelekezo pamoja na mapendekezo mbalimbali kuhusu namna ya kuinua kiwango cha shughuli hizo na kuimarisha nafasi ya madrasa hiyo katika nyanja za elimu na malezi.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alizungumzia falsafa ya kuanzishwa kwa madrasa hiyo na mfumo wake wa uongozi, akisema: “Kipindi fulani, Ofisi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu iliuliza kuhusu namna bora ya kuendesha madrasa hii. Wakati huo, mifumo kadhaa ya usimamizi ilipendekezwa, lakini hatimaye msisitizo uliwekwa katika kuifanya kuwa taasisi hai, yenye uchangamfu, inayotoa hamasa na yenye ushawishi katika shughuli za kitaaluma za Hawza.”
Akizungumza na viongozi wa Madrasat Imam Shahid, alisisitiza: “Ni muhimu kuunda jopo la ushauri na kikundi hai cha fikra ndani ya madrasa hii, kitakachokuwa kikifikiria na kupanga mara kwa mara kuhusu namna ya kujenga mazingira ya kiroho, kimaadili na yenye kutoa hamasa.
“Suala hili linahitaji usanifu wa jumla, tathmini endelevu na uboreshaji wa programu kwa kuzingatia misingi ya maadili na malezi ya Hawza. Ni lazima kuzingatia mila na desturi za Hawza, hususan zile ambazo zimejengeka kwa muda mrefu na wakati mwingine hurithishwa bila kuandikwa rasmi.”
Msisitizo wa Kiongozi Shahidi kuhusu mila na desturi zisizoandikwa za Hawza
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia misisitizo ya Kiongozi Shahidi kuhusu mila na desturi zisizoandikwa za Hawza, alisema: “Sehemu ya utambulisho wa Hawza imejificha katika mila na desturi hizi zisizoandikwa. Hizi ni desturi ambazo huenda isiwe rahisi kuzieleza kwa namna ya maagizo au kanuni zilizoandikwa, lakini kiutendaji zina nafasi muhimu katika kumlea mwanafunzi wa Hawza.”
Aidha, Ayatullah Arafi alisisitiza umuhimu wa kunufaika na uzoefu wa madrasaa na vituo vingine vya Hawza, kwakusema: “Katika masuala ya malezi na maadili, ni lazima kutumia fursa na uwezo uliopo, pamoja na kuweka ushirikiano wenye tija na vitengo vya utakaso wa nafsi na malezi katika Hawza.
Umuhimu wa kudhihirisha fikra za Mapinduzi ya Kiislamu kwa mtazamo wa hekima ndani ya Madrasat Imam Shahid
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran aliashiria kuimarisha fikra za Mapinduzi ya Kiislamu kuwa miongoni mwa majukumu muhimu ya Madrasat Imam Shahid (r.a.), akisema: “Moja ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika madrasa hii ni kudhihirisha fikra na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.”
Akisisitiza kuwa kuimarisha fikra hizo hakupaswi kusababisha kuwepo mipaka isiyo ya lazima au kugawanyika jamii katika makundi yanayopingana, alisema: “Lengo si kuanzisha mipaka ya kutenganisha watu ndani ya Madrasat Imam Shahid au kujenga mazingira ya makundi mawili yanayokinzana. Badala yake, roho ya fikra za Mapinduzi ya Kiislamu inapaswa kuwepo katika shughuli za kitaaluma, kiutamaduni na kimalezi za taasisi hii, kwa mtazamo wa kina, wa hekima, wenye utulivu na unaohifadhi heshima.”
Kujitokeza wimbi jipya la kuongezeka uelewa kuhusu fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na Muqawama duniani
Ayatullah Arafi, akizungumzia safari yake ya hivi karibuni nchini Bosnia na Herzegovina pamoja na baadhi ya mabadiliko ya kimataifa, alisema: “Duniani kumeanza kujitokeza wimbi jipya la kuongezeka uelewa na kuvutiwa na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na Muqawama. Wimbi hili, kwa baadhi ya mitazamo, linakumbusha mazingira yaliyokuwepo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hamasa kubwa ya tarehe 22 Bahman, isipokuwa kwamba leo limekuwa na kina na wigo mpana zaidi.”
Aliendelea kusema: “Katika mawasiliano na mikutano yangu ya kimataifa, hususan katika kipindi cha vita na mabadiliko ya hivi karibuni, nimekutana na wajumbe wa nchi za kigeni wapatao 200 hadi 300. Pia, katika safari mbili nilipata fursa ya kushuhudia moja kwa moja kiwango cha mapokezi mazuri na hamu iliyopo ya kutaka kufahamu fikra za Mapinduzi ya Kiislamu. Kiwango hiki cha kuvutiwa na fikra hizo miongoni mwa baadhi ya wananchi na wasomi wa nchi mbalimbali kinastahili kuzingatiwa kwa kina.”
Fiqhi ya kisasa iwe miongoni mwa mihimili hai ya kitaaluma ya madrasa
Katika kuendelea na hotuba yake Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alizungumzia msisitizo wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu nafasi ya Fiqhi na elimu ya Fiqhi katika madrasa hii, akisema: “Kama ilivyosisitizwa pia katika kipindi cha kuanzishwa taasisi hii, moja ya mihimili mikuu ya shughuli za madrasa inapaswa kuwa Fiqhi na elimu ya Fiqhi. Mwelekeo huu unapaswa kuendelea kufuatiliwa kwa nguvu ileile.”
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alisisitiza pia jambo muhimu kwamba, sambamba na kuhifadhi utambulisho na mbinu za jadi za Hawza katika taaluma ya Fiqhi, ni lazima kuweka mipango yenye busara na ya kitaaluma ili kuzingatia mijadala mipya na masuala yanayoibuka katika zama hizi. Hii ni kwa sababu Fiqhi inapaswa kuwa na uwezo wa kutoa majibu kwa mahitaji yanayobadilika ya jamii na changamoto mpya za ulimwengu wa sasa.
Kufanyika darsa 100 za maandalizi ya Fiqhi ya kisasa
Ayatullah Arafi, akizungumzia kuanzishwa mkondo wa Fiqhi ya kisasa katika Hawza, alisema: “Takribani miaka saba iliyopita, katika kikao kimoja na Marji' Taqlid mkubwa, tulizungumzia suala la kuanzisha mkondo wa Fiqhi ya kisasa. Leo, juhudi hizo zimezaa matunda ya takribani vitabu 70 na karibu darsa 100 za maandalizi ya Fiqhi ya kisasa.”
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, akieleza kuwa harakati hii ya kitaaluma imegeuka kuwa mkondo hai unaoendelea kupanuka, aliongeza: “Harakati hii ina uwezo wa kupanuka zaidi katika mwaka ujao, na inatarajiwa kuwa idadi kubwa ya darsa na programu zake itaongezeka.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala mapya yanayoibuka katika eneo hili, alisema: “Masuala kama vile akili unde (Artificial Intelligence) na changamoto nyingine mpya za kitaalamu zinazojitokeza katika nyanja mbalimbali zinapaswa kuwa miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika tafiti za Fiqhi.
“Katika suala hili, baadhi ya wataalamu na watu walioshiriki katika darsa hizi wanakiri kwamba mijadala hiyo imeandaliwa kwa namna inayowezesha kuchunguza kwa usahihi vipengele na pande mbalimbali za masuala mapya.”
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza alisisitiza: “Madrasa ya Imam Shahid (r.a.) nayo inapaswa kuingia katika uwanja huu kwa bidii na kwa mtazamo makini, huku ikihifadhi misingi ya kitaaluma na mila halisi za Fiqhi, ili iwe moja ya vituo vikuu vya kitaaluma vinavyoshughulikia uchunguzi wa masuala mapya ya Fiqhi.
Maoni yako